KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kujiuzulu uenyekiti kwa kile alichosema amekiaibisha chama kwa hukumu aliyopewa hivi karibuni.

Mbowe alihukumiwa hivi karibuni kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini
ya Sh milioni moja baada ya kutiwa hatiani na mahakama mkoani
Kilimanjaro kwa kosa la kumpiga Msimamizi wa Uchaguzi mwaka 2010.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Karumwa, wilayani
Nyang’hwale mkoani Geita, Nape alisema miongoni mwa sifa za kiongozi, ni
kuzuia hasira na kuwa na kifua kigumu.
Alisema kwa kulinda heshima yake na ya chama chake, Mbowe anapaswa kujiuzulu.
“Jana (juzi) Mahakama ya Hai mkoani Kilimanjaro ilitoa hukumu ya
kumfunga jela mwaka mmoja Mbowe au alipe faini ya Sh milioni moja. Yeye
na chama chake waliamua kulipa faini ili asiende jela,” alisema Nape.
Akisisitiza kuwa alichofanya Mbowe ni aibu, Nape alisema, “mtu mzima
ukiwa umejifunga taulo na mtoto akaja kuichukua hutakiwi kumkimbiza
mtoto badala yake unatakiwa kuchutama.
“Ukiamua kumkimbiza mtoto na wewe unaonekana akili yako kama mtoto. Yeye
ni kiongozi wa chama, alitakiwa kuonesha uwezo wake kama kiongozi,
kutumia hekima na busara dhidi ya msimamizi huyo wa uchaguzi badala ya
kumpiga hadharani.”
0 comments:
Post a Comment