SOMA HISTORIA YA SHUJAA HUYU WA BONGO FLEVA ALIYESAHAULIKA
JAMES Dandu ‘Mtoto wa Dandu’ siyo jina geni katika gemu la Bongo
Fleva lakini ni wangapi wanamkumbuka na wanautambua mchango wake katika
gemu la Bongo Fleva? Ungana nami ili kumjua kwa kina.
James Dandu ‘Mtoto wa Dandu’ (kushoto katika picha) enzi za uhai wake.
HISTORIA YAKE KWA UFUPI ALIVYOINGIA KWENYE GEMU
James Dandu au kwa jina
lingine Cool James Massive ‘CJ Massive’ alizaliwa Julai 5, 1970, Mwanza
nchini Tanzania. Alisoma shule ya Msingi Kurasini na baada ya hapo,
yeye, mama yake na ndugu zake walihamia jijini Stockholm, Sweden
alikoishi kwa kipindi kirefu.
James Dandu aliingia
rasmi kwenye sanaa ya muziki mwaka 1988 akiwa jijini Stockholm ambapo
alitoa singo kadhaa zikiwa katika staili ya Euro-House. Mwaka 1992
aliachia albamu yake ya kwanza ambayo hata hivyo haikupata mafanikio
makubwa.
Mwaka 1993, aliungana na msanii mwingine kutoka Afrika Mashariki,
Andrew Muturi na kuunda kundi lililokwenda kwa jina la Swahili Nation.
Wasanii wengine wawili wakajiunga kwenye kundi hilo.
Baadaye, James
Dandu alijitoa kwenye kundi hilo na kuungana na Mkongomani, Jose Masena
‘Black Teacher’ na kutoa albamu mbili zilizowatambulisha vyema sehemu
mbalimbali; Undercover Lover (1992) na Zooming You (1995) iliyokuwa na
wimbo ulioitwa Dr. Feel Good. Wakapata mafanikio makubwa na kuingiza
mkwanja wa maana.
AREJEA BONGO KWA KISHINDO
Kutokana na mafanikio
makubwa aliyoyapata akiwa na mwenzake, Black Teacher, Mtoto wa Dandu
aliamua kurudisha majeshi nyumbani kwa lengo la kuja kuibua na kuinua
vipaji Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.
Aliporudi Bongo, alikuja na staili mpya ya uimbaji wa nyimbo za
taratibu (R&B) ambao haukuwa umezoeleka sana kwa kipindi hicho.
Akajipatia umaarufu mkubwa ndani ya kipindi kifupi.
Hakuishia hapo,
aliendelea kuingiza ubunifu katika kazi zake, akawa anachanganya R&B
ya kisasa, Rhumba na Ndombolo (staili iliyokuwa maarufu sana nchini
Zaire kipindi hicho). Akatoa albamu nyingine kama Soft Like a Pillow
(1997), Bi Harusi (1998) na Sukuma Land (2002).
Miongoni mwa ngoma ambazo mpaka leo zikipigwa lazima watu watulie ni
Sina Makosa ambayo aliurudia wimbo wenye jina hilohilo uliopigwa na Les
Wanyika kutoka Kenya. Ngoma hii ilimtambulisha kinoma Afrika Mashariki
yote, hususan nchini Kenya.
Pia alifanya remix ya wimbo wa Mamu akiwa na mkali Madilu System ambao ama kwa hakika ulibamba mbaya!
TUZO ZA KILI
Mwaka 1999, James Dandu aliamua
kuanzisha tuzo alizoziita Tanzania Music Awards ambazo hivi sasa
zinajulikana kama Kili Music Awards baada ya kuanza kudhaminiwa na bia
ya Kilimanjaro.
James Dandu ndiye aliyefanikisha usajili wa tuzo
hizo kwa kushirikiana na Basata chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni
(kipindi hicho).
KIFO CHAKE
Mtoto wa Dandu alifariki Agosti 27,
2002, kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Makumbusho jijini Dar es
Salaam, nyota yake ikiwa inang’ara kinoma na kuzusha simanzi kubwa
miongoni mwa mashabiki wake, hususan wanawake ambao walikuwa mashabiki
wake wakubwa.
Akaenda kuzikwa nyumbani kwao, Mwanza. Wakati anakufa, alikuwa bado
hajamaliza kurekodi kazi zake mpya katika Studio ya Master Jay. Aliacha
watoto wawili wakiwa bado wadogo pamoja na mjane, Devotha.
MIAKA 12 BAADA YA KIFO CHAKE
Ni miaka 12 sasa
imepita tangu Mtoto wa Dandu aliporejea kwenye makazi yake ya milele.
Swali ambalo mimi na wewe tunapaswa kujiuliza, je, anapewa heshima
anayostahili hata kama alishatangulia mbele za haki? Familia yake
wakiwemo wanaye Caroline-Jamie ’Malaika’ aliyezaliwa mwaka 1994 na
Michael James Junior aliyezaliwa 1997 wananufaika na matunda ya kazi za
baba yao? Nawashauri waandaaji wa Tuzo za Kili wamuenzi James Dandu japo
kwa tuzo ya heshima!
0 comments:
Post a Comment