MSANII 20 PERCENT AKUTWA KWA MGANGA WA KIENYEJI AKIFANYA YAKE
Abas Kinzasa ‘20%’.
Stori: Musa Mateja na Shakoor Jongo
Makubwa! Kichwa cha Bongo Fleva kutoka pande za Kimanzichana mkoani
Pwani, Abas Kinzasa ‘20%’, anadaiwa kunaswa laivu akiwa kwa mganga wa
kienyeji akipata tiba ya kupunguza na kuondoa sumu ya utumiaji wa bangi
na pombe
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, ishu hiyo ilijiri katika Kijiji
cha Ngukumo mkoani Tabora baada ya mameneja wa wasanii wa Bongo Fleva,
Papa Misifa na Steve Mbaga kumshika mkono 20% na kutafuta mganga wa
kienyeji ambaye aliwatangazia kuwa ana dawa zinazoweza kumuondoa sumu
hiyo.
Baada ya kunyetishiwa stori hiyo, gazeti hili liliwatafuta mameneja
hao ambao walisema walilazimika kufanya hivyo ili waweze kumrudisha 20%
kwenye gemu kwa mara nyingine kwani bado wanaamini ana uwezo mkubwa
kwenye muziki wa Bongo Fleva.
“Kiukweli mimi na mwenzangu tumekuwa tukisikitishwa kwa muda mrefu
baada ya 20% kubobea kwenye matumizi ya pombe na bangi na hasa
alipozidiwa hadi akashindwa kufanya muziki huu ambao tunaamini kwake
ndiyo ilikuwa ajira pekee.
“Kwa kutambua hilo tulimtafuta na kuongea naye, alipokubaliana nasi
tukaamua kumpeleka kwa mganga wa kienyeji, ameshapata tiba na tayari
ameonyesha kujitambua, hivyo hivi karibuni tunaanza kufanya naye kazi na
ndiyo tunatoka kumlipia nyumba ya kuishi maeneo ya Mwananyamala
Hospitali,” alisema Papa Misifa.
Ijumaa Wikienda lilimtafuta 20% ambaye mwaka 2011 alichukua tuzo tano
za Kili na kumuuliza juu ya suala hilo ambapo alikuwa na haya ya
kusema: “Ni kweli Papa Misifa na Steve Mbaga wamejitahidi sana kunifanya
niachane kabisa na matumizi ya pombe maana walinipeleka kwa mganga wao
ambaye kweli amenisaidia.
“Ujue kilichokuwa kikiniyumbisha siku zote hizo ilikuwa ni pombe
maana bangi ilikuwa si kiivyo, nilipokuwa nakunywa pombe kweli ilikuwa
ikinitoa kwenye njia na kunifanya kujiona mimi ndiyo mimi kiasi cha
kushindwa hata kuwaheshimu wenzangu na ndiyo jambo pekee ninaloweza
kusema limenifanya kuwa hivi.”
chanzo: Ijumaa Wikienda
0 comments:
Post a Comment