Watu watano wafariki dunia katika Mapigano ya wakulima na wafugaji wa mipaka ya Shinyanga na Tabora
Mapigano ya kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji katika eneo la mpaka kati ya wilaya za Kishapu mkoani Sninyanga na Igunga, mkoani Tabora yameua watu watano.
Mapigano hayo yaliyotokea Jumapili iliyopita katika kijiji cha Magalata
wilayani Kishapu na kusababisha vifo hivyo na mtu mmoja kujeruhiwa baada
ya kushambuliana kwa kutumia mikuki.
Waliouawa ni Peter Korongo Masolwa(72) Chawalwa Duke(50) Diblo Kingu(50)
Mohamed msengi(40) Kende Doma(70) wakazi wa Kishapu na Igunga.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilison Nkhambaku, alisema mapigano hayo
yalitokea eneo la Magogo na kwamba wafugaji wa jamii ya Kitaturu
walinyang’anywa na wakulima mifugo yao zaidi ya ng’ombe 3,000 ambazo
ziliswagwa na kupelekwa wilayani Igunga.
Nkhambaku alisema kutokana na tukio hilo, ilibidi kamati ya ulinzi na
usalama wa wilaya zote mbili Kishapu na Igunga walikaa kikao na
kulijadili suala hilo kwa kulitafutia ufumbuzi, na kuwa waliwataka
wafugaji na wakulima kuacha mapigano hayo ikiwa serikali inalitafutia
ufumbuzi pamoja na kutenga maeneo ya kilimo na sehemu za machungo ya
mifugo.
Baadhi ya wafugaji walisema mapigano hayo yalitokana na wakulima kulima
mazao maeneo yote na kusababisha kukosa maeneo ya malisho, hivyo kuamua
kutafuta haki yao kwa nguvu.
Mmoja wa wafugaji hao, Ndelanha Mahona, alisema ng’ombe zaidi ya 3,000
waliswagwa na kupelekwa Igunga, kitendo ambacho wafugaji hawakukubali na
kusababisha mapigano hayo.
Wakulima walidai wafugaji hao wamekuwa wakipitisha mifugo yao katika
mashamba na kulisha mazao yao, kitendo ambacho hawakukubaliana nacho
kwa kuwasababishia hasara kila mwaka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu, Justin Sheka, alisema mapigano
hayo yamehatarisha amani kwa wananchi, huku akiwataja walionyang’anywa
mifugo hiyo kuwa ni Ndelanha Mahona, Mbuta Madila, Silag’wan Hendeka,
Gidi Babashi na Gilijisiji Gilawida ambaye alijeruhiwa kwa kuchomwa
mkuki.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu, Shija
Ntelezu, aliitaka serikali kulitafutia ufumbuzi suala hilo haraka
kutokana na wananchi kuanza kuuana hovyo.
“Suala hili linahitaji ufumbuzi wa haraka, eneo hilo la Mbuga ya
Magalata lilitengwa kwa ajiri ya machungio ya mifugo, lakini wakulima
wamevamia eneo hilo wakidai na wao wana haki ya ardhi na kuanza kulima
mazao, hivyo serikali haina budi kulitatua tatizo hilo haraka ili
kuepusha mauaji,” alisema Ntelezu.
Kufuatia mapigano hayo, wakuu wa mikoa ya Tabora na Shinyanga wameunda timu ya watu 18 kuchunguza chanzo cha mgogoro huo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Nasoro Rufunga na Mkuu wa Mkoa wa
Tabora, Fatuma Mwasa, walisema wameazimia kuwa wafugaji wa Kishapu
wabaki katika eneo lao la Magalata wasivuke mto Manonga.
Walisema pia kwamba wakulima wa Igunga walioko katika vijiji vya Magogo
na Isakamaliwa wabaki katika vijiji vyao na wasivuke mto Manonga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala, alisema msako unaendelea kuwabaini waliohusika na mapigano hayo.
0 comments:
Post a Comment